SANA: Asasi yenye mwarobaini wa kutokomeza uharibifu wa mazingira
· Badala ya kukata miti, yawafundisha wananchi kutengeneza mkaa wa mabua
Na Daniel Mbega
SUALA la kuhifadhi mazingira limekuwa moja ya ajenda zinazopewa kipaumbele katika mikutano na makongamano mengi kote ulimwenguni kwa sasa kutokana na ukweli kwamba mazingira yanaharibiwa kila siku na binadamu hao hao wanaoyahitaji kwa ustawi wa maisha yao.
Uharibifu wa mazingira umezikumba nchi nyingi duniani, lakini umekuwa na athari kubwa sana hasa kwa nchi za dunia ya tatu au zinazoendelea, Tanzania ikiwa miongoni mwazo.
Inaelezwa kwamba tabaka la anga, maarufu kama Ozone Layer, limeharibika vibaya kutokana na kemikali nyingi zinazozalishwa katika nchi zilizoendelea na zenye viwanda vingi, kiasi kwamba kwa miaka ya karibuni hata hali ya hewa imebadilika ambapo mvua hazinyeshi kwa kiwango kinachotakiwa na joto limezidi sana duniani.
Lakini, pamoja na viwanda hivyo kuharibu mazingira, pia ukataji wa miti umekuwa chanzo kikubwa cha nchi nyingi kugeuka jangwa huku vyanzo vya maji navyo vikiathirika kwa kiwango kikubwa, kwani hata baadhi ya chemchem zilizokuwepo tangu zama zimeshakauka.
Milima mingi nayo imebaki na vipara vya hapa na pale huku misitu, hasa ile ya asili, ikiondolewa kwenye uso wa dunia kutokana na kukatwa miti kunakofanywa na binadamu.
Aidha, ukataji huo wa miti na uharibifu wa mazingira kwa ujumla – ya nchi kavu na hata majini – umesababisha viumbe hai wengi wakiwemo samaki, ndege na wanyama wa porini kutoweka katika ramani ya ulimwengu.
Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi za asili – ardhi yenye rutuba, misitu na wanyama – lakini ukizunguka kwa sasa unaweza kushangaa kuona maeneo yale yaliyokuwa na misitu takriban miaka 10 iliyopita yamegeuka kuwa nusu jangwa kutokana na kutokuwepo na hata mti mmoja wa asili, achilia mbali miti ya kupandwa.
Hii inatokana na ukweli kwamba, binadamu ameyaharibu mazingira mengi yanayomzunguka na kama juhudi za makusudi hazitafanyika, Tanzania itakuwa jangwa katika miaka michache ijayo.
Sababu kubwa zinazochangia ukataji wa miti ni za kiuchumi na kijamii. Ukizunguka katika sehemu kubwa ya kaskazini mwa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, na kusini mwa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, utakuta eneo kubwa la misitu limefyekwa kwa sababu za kiuchumi. Wanaofanya hivyo, wengi wanataka maeneo ya kilimo.
Ukiacha shughuli hizo za kilimo, sehemu nyingine miti inakatwa kwa ajili ya matumizi ya kijamii, hususan nishati ya kuni na mkaa. Ni shughuli za kijamii, lakini zinazoambatana na kiuchumi, kwani kuni na mkaa huo unauzwa na wahusika ili kujipatia fedha za kuendesha maisha yao.
Lakini je, hivi hakuna njia mbadala ya kujipatia fedha kuliko kukata miti hii ambayo ni chanzo kikubwa cha mvua? Hili ndilo swali linalojibiwa na Angela Damas, Miss Tanzania wa mwaka 2002, ambaye kwa sasa ni Meneja Miradi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Saving Africa’s Nature (SANA).
Angela anasema inawezekana kabisa kupata njia nyingine mbadala ya kuwawezesha Watanzania kupata nishati na kipato pia, ndiyo maana wao SANA wameamua kuja na mradi wa Mkaa kwa Njia Endelevu (Sustainable Charcoal Project) ambao siyo tu unajali, kutunza na kuyaendeleza mazingira, lakini pia unawawezesha wananchi wenyewe kuyapenda na kuyahifadhi zaidi kwa manufaa yao wenyewe na vizazi vijavyo.
“Mradi huu hauhitaji kukata mti hata mmoja, zaidi tunahimiza upandaji wa miti na pia kuitunza ile iliyopo kwa faida yao na vizazi vijavyo,” anasema Angela ambaye taasi yake imesajiliwa rasmi Novemba 2008.
Anasema kwa kupitia progamu hiyo, wanahimiza wananchi kutotumia miti kupata nishati ya mkaa, badala yake wanatumia taka shamba – mabua na taka nyingine laini – ambazo huzichoma kwenye kinu maalum na kisha kusindika majivu yake ambayo matokeo yake yanatoa mkaa ulio bora kuliko hata ule unaotokana na kuchoma miti.
“Mabua yanakusanywa na kushindiliwa kwenye mapipa ya kawaida yaliyo wazi, halafu mapipa haya yanaingizwa kwenye pipa maalum ambapo yanachomwa. Baada ya hapo majivu yanayopatikana yanachanganywa na kusindikwa kwa kutumia kinu kidogo kutoa mabonge ya mkaa tayari kwa matumizi,” anasema Angela.
Angela anasema kwamba, tayari teknolojia hii mpya wameianzisha katika kijiji cha Mkange wilayani Bagamoyo, Pwani ambacho kwa kiasi kikubwa kimeathirika kutokana na ukataji miti kwa nia ya kuchoma mkaa.
“Kijiji cha Mkange biashara yake kubwa ni mkaa, hivyo kimeathirika mno kutokana na misitu mingi kukatwa kwa lengo la uchomaji wa mkaa. Awali tulipoingia na wazo hili ilionekana kama elimu ngeni na wengi waliipuuza, lakini kwa sasa tunashukuru kwamba tumeshaokoa miti mingi na tayari wananchi wanaichangamkia teknolojia hii kwa kuchoma mkaa huu.
“Wanajipatia pesa, lakini pia inawasaidia kusafisha mashamba yao kwa njia ya faida. Kama zamani walikuwa wakikusanya taka za shamba na kuzichoma moto ovyo, leo hii hawataki mtu mwingine aingie mashambani mwao kukusanya mabua, wanayakusanya wenyewe na kuyachoma kisha kutengeneza mkaa ambao wanauza na kujipatia kipato,” anasema kwa tabasamu.
Aidha, anasema taasisi yao ambayo siyo ya kibiashara, inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa fedha ili kuifikisha elimu hiyo katika sehemu kubwa ya Tanzania, kwani zaidi wanategemea wahisani ili kufanikisha azma hiyo.
“Kwa kupeleka elimu katika eneo moja tunahitaji Dola za Marekani 650 ambazo tunazitumia kwa ajili ya kununulia kitu maalum cha kusindika mkaa pamoja na gharama za mafunzo. Elimu hii tunayo na tunataka imfikie kila mwananchi kwa lengo la kumsaidia kupata fedha na kuokoa mazingira yasiharibiwe huku tukiwahimiza wapande miti kwa wingi,” anaongeza.
Wazo hili lilitoka wapi? Angela anasema wazo la kuanzisha miradi kama hiyo lilitoka kwa Costas Coucolis, Mkurugenzi Mkuu wa Saadani Lodge ambaye aliona teknolojia hiyo katika nchi nyingi zilizoendelea.
Awali walianza kutoa misaada tu kwa jamii, lakini baadaye wakaamua kujisajili rasmi ili watambulike hata kimataifa kwa lengo la kuhimiza utunzaji wa mazingira. Mkurugenzi wake ni Marianna Balampama, ambaye anaonekana kuwa mwenye uchungu na jinsi mazingira yanavyoharibiwa ulimwenguni.
Malengo yao makubwa ni kuhimiza na kuendesha programu zinazoweza kuwa njia mbadala ya nishati kwa jamii, kuendesha shughuli za uzalishaji mali zinazoweza kuwafaa wanajamii katika sekta za elimu, afya na maendeleo kwa ujumla, kuimarisha uelewa wa jamii kwa kuyatambua mazingira yao na viumbe vilivyomo, kuwajengea uwezo wanajamii kukabiliana na kupambana na umaskini kwa kuzingatia miongozo ya Mpango wa Kukuza Uchumi na Kutokomeza Umaskini (Mkukuta) na mipango na sera zingine.
Kwa sasa SANA inaendesha programu zake katika vijiji kadhaa; Saadani, Mkange, Kijiji cha Maasai huko Miono, na Gongo – Matipwili, vyote vikiwa katika wilayani ya Bagamoyo mkoani Pwani, lakini malengo yake makubwa yakiwa kusambaza teknolojia na elimu ya uanzishaji wa miradi mbalimbali nchini kote.
“Ni taasisi ya kujitolea, hivyo kila mmoja wetu anajitahidi kutimiza wajibu wake katika miradi ambayo tayari tunaisimamia kama elimu, afya na teknolojia. Tayari SANA inafadhili wanafunzi 10 kutoka Saadani wanaosoma sekondari na mmoja anayesoma Shule ya Sekondari Matipwili,” anasema mratibu wa SANA, Ally Abdallah.
Anaongeza: “Tunatarajia kujenga zahanati katika Kijiji cha Gongo ambayo itakuwa na wodi ya wazazi ili kuwaokoa wanawake kutokana na vifo vinavyotokana na uzazi, kuanzisha ushirika katika Kijiji cha Maasai cha Msete, na tutajenga kituo vya kujipatia fedha katika Kijiji cha Mseni ambayo itamilikiwa na wananchi wenyewe.”
Lakini, mbali ya hayo, Angela kwa upande wake anasema wanawake wanapewa msukumo kwenye programu zao ambapo tayari wamefunzwa na kuwezeshwa kuanzisha miradi mbalimbali, hususan wa bustani ili kujipatia kipato.
“Iko mipango mingi inayohitaji uwezeshwaji. Tuna mradi wa matumizi ya gesi asilia (Bio gas), ambapo tayari Saadani Lodge na Shule ya Sekondari ya Azania, Dar es Salaam wanatumia…
…Tuna mpango wa kuhamasisha na kuelimisha kuhusu teknolojia ya umeme-jua, yote hii inahitaji uwezeshwaji, ingawa sisi kama watendaji tuko tayari. Yeyote mwenye nia thabiti ya kuokoa mazingira yetu tunaomba atuunge mkono kwa kutoa mchango wake ili kutuwezesha tutende kazi,” anaongeza Angela.
Lakini, kila kitu kinawezekana ikiwa Watanzania wataamua kuwaunga mkono SANA na taasisi zingine ambazo zimekuwa mstari wa mbele kuyatunza mazingira yasiharibiwe kwa kiasi kikubwa kwa kisingizio cha kutafuta mapato.
Idadi kubwa ya wananchi, hasa wale wa vijijini wakipata elimu ya kutunza mazingira na hasa kuwaelimisha njia mbadala ya kuacha kukata miti kwa ajili ya mkaa au kuni kwa kuwapa elimu kama inayotolewa na SANA.
Nishati mbadala ni ngao muhimu kwa kutunza miti na hatimaye mazingira yote kwa neema ya vizazi vya sasa na baadaye.
Elimu ya kutengeneza mkaa kwa taka za shamba ni mwokozi wa mazingira yetu, hivyo kila mmoja awajibike. Inawezekana
Ends

No comments:
Post a Comment